Kila nambari ina maana muhimu
Tumeandaa dondoo 30 muhimu zitakazokusaidia kuelewa ukubwa wa changamoto na fursa za kuchukua hatua.
November 10, 2025
Mabadiliko ya tabianchi yanaathiri kila nyanja cha maisha yetu. Tumeandaa dondoo 30 muhimu zitakazokusaidia kuelewa ukubwa wa changamoto na fursa za kuchukua hatua.
Jifunze takwimu zinazoeleza changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kwa nini kila uamuzi tunaouchukua una umuhimu mkubwa.
Kuna sayari 1 inayoweza kuendeleza uhai wa dunia.
Uwezo wa sayari yetu kuendeleza uhai ni matokeo ya mambo kadhaa, yakiwemo wingi wa maji, uga wa sumaku unaolinda dhidi ya miale hatari ya jua, na joto la wastani linalodhibitiwa na angahewa yenye tabaka la kuhifadhi joto.
Lakini, mabadiliko ya tabianchi, yanayosababishwa na gesi joto zinazotokana na shughuli za kibinadamu, yanasababisha Dunia kupata joto kwa kasi isiyo ya kawaida. Hali hii inavuruga uwiano tete unaodumisha uhai, ikileta madhara makubwa kwa viumbe na kuhatarisha jamii.
Je, wajua: Nchi tajiri zinatumia rasilimali za Dunia kwa viwango ambavyo vingehitaji Dunia kati ya 3 hadi 9 ili kumudu. Ili kuzuia mabadiliko ya tabianchi na kulinda mustakabali wetu, ni lazima tubadilike.
Kupitia Mkataba wa Makubaliano Paris, nchi zilikubaliana kudhibiti ongezeko la joto duniani lisiwe zaidi ya nyuzi 2°C, huku zikijitahidi kulizuia lisizidi 1.5°C.
Mnamo mwaka 2015, mataifa yalifikia makubaliano ya kihistoria na kupitisha mkataba huu wa makubaliano wa Paris, ambao umebaki kuwa msingi wa hatua za dunia nzima kubabiliana and ujiwezessha dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Mkataba wa Makubaliano wa Paris ulikuwa mkataba wa kwanza wa kimataifa uliotaja wazi kikomo cha ongezeko la joto duniani, ambapo nchi zilikubaliana kushirikiana ili kudhibiti ongezeko la joto duniani lisizidi nyuzi 2°C, huku zikijitahidi kulizuia lisipite nyuzi 1.5°C.
Wanasayansi wanaonya kuwa kudhibiti ongezeko la wastani wa joto duniani lisizidi 1.5°C juu ya viwango vya kabla ya mapinduzi ya viwanda ni jambo muhimu sana ili kuepuka madhara mabaya zaidi na kuvuka viwango vya hatari visivyoweza kurekebishwa.
Je, wajua: Kila ongezeko dogo la joto linaongeza hatari na madhara makubwa ya hali ya hewa. Kwa mfano, katika ongezeko la 1.5°C, takribani asilimia 14 ya watu duniani watakumbwa na joto kali kila baada ya miaka mitano. Katika 2°C za joto, idadi hiyo huongezeka hadi asilimia 37, au takribani bilioni 1.7.
Mabadiliko ya tabianchi yanaathiri kila mtu, lakini zaidi ya watu bilioni 3 wanaishi katika maeneo hatarishi.
Mabadiliko ya tabia nchi yanaleta athari katika jamii, ikiwa ni pamoja na hali mbaya zaidi ya anga, inayoleta upungufu wa chakula, madhara ya kiafya, na hasara zisizoweza kurekebishwa.
Ingawa kila mtu duniani ameanza kuona athari zake, baadhi ya nchi zinaathirika zaidi kutokana na eneo lao kijiografia, uwezo wa kiuchumi na uwezo mdogo wa kukabiliana na hali hiyo. Kati ya watu bilioni 3.3 hadi 3.6 wanaishi katika maeneo hatarishi, hasa barani Afrika, Asia Kusini, Amerika ya Kati na Kusini, visiwa vidogo, na Aktiki.
Je, wajua: Changamoto za mabadiliko ya tabianchi hayana uwiano wausawa, nchi maskini zinaathirika zaidi. Nchi hizi zinaathirika mara nane zaidi na majanga yanayohusiana na hali ya hewa kuliko miaka 30 iliyopita, na madhara ya kiuchumi yameongezeka mara tatu.
Afrika inazalisha chini ya asilimia 4 ya gesi joto duniani, lakini athari za mabadiliko ya tabia nchi ni kubwa zaidi barani humo.
Hili ni suala la haki za kijamii. Watu na jamii zinazoathirika zaidi na adha ya mabadiliko ya tabia nchi mara nyingi sio zinazochangia katika uharibifu huu.
Nchi za Afrika zinazalisha chini ya asilimia 4 ya gesi joto duniani, lakini athari za mabadiliko ya tabia nchi ni kubwa zaidi na zinaathiri kila nyanja ya maendeleo, inachochea njaa, usalama na watu kuhamahama.
Nchi na sekta ambazo zimepata utajiri kutokana na uzalishaji mkubwa wa gesi joto zina wajibu wa kupunguza uzalishaji kwa kasi na kusaidia wale wanaoathirika zaidi.
Je, wajua? Hata ndani ya nchi moja, athari za mabadiliko ya tabianchi hujitokeza kwa viwango tofauti kutokana na tofauti za kijamii, kabila, jinsia, umri na hadhi ya kiuchumi.
Kila baada ya miaka 5 nchi zina wasilisha mipango thabiti ya kitaifa ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuonyesha dhamira yao ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mkataba wa Makubaliano wa Paris huwa ni wa miaka mitano unaochochea maamuzi chanya kuhusu mabadiliko ya tabia nchi. Nguzo muhimu ya kukabiliana na changamoto hii ni Mipango thabiti ya kitaifa ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Mipango hii ya nchi inaainisha jinsi nchi zilivyojipanga kupunguza uzalishaji wa gesi joto na kukabiliana na athari zake.
Mipango hii inasaidia nchi kuainisha malengo na hatua muhimu za kuchukua kwenye sekta muhimu kama nishati, kilimo, maji, afya, miundombinu na usafiri. Kwa kurekebisha mipango hii, kila baada ya miaka mitano, nchi zinaweza kuelekeza uchumi wao katika njia ya kufikia kutokuwa na uzalishaji kaboni ifikapo 2050.
Je, wajua: Kizazi cha kwanza cha hii mipango, kiliweka dunia katika njia ya ongezeko la 3.7°C, kizazi cha pili kikipunguza hadi 2.7°C, na kizazi cha tatu kinatarajiwa mwishoni mwa mwaka 2025, kikihimizwa kulingana na kikomo cha 1.5°C.
Athari za mabadiliko ya tabianchi ni kubwa mara 6 zaidi ya kufikia malengo yaliyoanishwa kwenye Mkataba wa Makubaliano wa Paris.
Madhara ya mabadiliko ya tabia nchi yanayoonekana sasa yanaweza kuathiri Uchumi wa dunia kwa asilimia 19 ifikapo mwaka 2050.
Madhara haya kwenye mavuno, uzalishaji, na miundombinu zinakadiriwa kufikia dola za Marekani trilioni 38 — mara sita zaidi ya gharama zinazohitajika kupunguza ongezeko la joto duniani hadi nyuzi 2°C.
Je, wajua: Gharama halisi za athari za mabadiliko ya tabianchi zimekuwa zikikadiriwa chini ya uhalisia kwa miongo kadhaa. Utafiti mpya unaonyesha kuwa hasara za kiuchumi ni kubwa zaidi kuliko ilivyotabiriwa awali.
Bila kuchukua hatua za dharura za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kizazi cha sasa kitaathirika na mabadiliko haya mara 7 zaidi ya kizazi kilichopita.
Kwa sababu ya maamuzi yaliyofanywa ya vizazi vilivyopita, haki za watoto na vijana ya kuwa na makazi salama, mazingira yenye afya, elimu bora, chakula, na huduma za afya, iko katika hatari kwa sababu ya athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kadri wanavyokua, watoto na vijana watabeba mzigo mkubwa wa athari za mabadiliko ya tabianchi kama vile joto kali, mafuriko, misitu kuwaka moto na udumavu wa mazao. Hii inaleta changamoto za usawa kati ya kizazi cha sasa na kilichopita, jambo lililochochea harakati zinazoongozwa na vijana duniani kote, kesi kuhusu mabadiliko ya tabianchi, na juhudi za kushughulikia athari za kiusalama zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi.
Je, wajua: Watoto wanaoishi katika nchi maskini au jamii zenye mazingira duni wako katika hatari kubwa zaidi. Kwa mfano, nchini Afghanistan, watoto wanaweza kukumbwa na joto kali mara 18 zaidi ya wazee wao, huko nchini Mali, wanaweza kukumbwa na hali hiyo mara 10 zaidi pamoja na kudumaa kwa mazao yao.
Watu 8 mpaka 10 wanatamani serikali zao ziweke jitihada zaidi katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi
Mchango mkubwa wa maoni ya watu kuhusu mabadiliko ya tabianchi umeonyesha kuwa asilimia 80 ya watu duniani wanataka serikali zao zichukue hatua thabiti kukabiliana na changamoto hii.
Aidha, asilimia 86 wanaunga mkono nchi zao kuacha tofauti za kisiasa na kijiografia (kama vile biashara na usalama) na kushirikiana kwa pamoja katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Je, wajua: Duniani kote, asilimia 72 ya watu wanaunga mkono maamuzi ya haraka kutoka matumizi ya nishati ya mafuta kwenda kwenye nishati mbadala. Hata katika nchi wazalishaji wakubwa wa mafuta na makaa ya mawe, wananchi wengi wanaunga mkono mabadiliko haya.
Uchumi wa kijani unachangia kwa takribani asilimia 9 ya masoko ya mtaji duniani
Uchumi wa kijani unakua kwa kasi. Kadri nchi zinavyojaribu kukabiliana na changamoto za kimazingira, sekta kama uzalishaji wa nishati mbadala, miundombinu endelevu, usimamizi wa taka, udhibiti wa uchafuzi wa mazingira, na kilimo cha kisasa vinaendelea kupanuka.
Kwa sasa, thamani ya uchumi wa kijani inakadiriwa kufikia dola za Marekani trilioni 7.9, ikiwakilisha takriban asilimia 9 ya hisa zote zinazouzwa duniani.
Je, wajua: Katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, thamani ya hisa za sekta ya kijani imekua kwa kiwango cha wastani wa asilimia 15 kwa mwaka, ikiifanya kuwa sekta ya pili inayokua kwa kasi zaidi duniani baada ya teknolojia.
Kila dola 1 inayowekezwa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi inaweza kutoa faida ya dola 10 katika kipindi cha miaka 10.
Kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ni muhimu ili kupunguza hatari na kuongeza ustahimilivu wa jamii na mifumo ya ikolojia.
Kila dola 1 inayowekezwa katika hatua za kukabiliana inaweza kutoa faida za zaidi ya dola 10 katika kipindi cha miaka 10, kwa kuepuka hasara, kuchochea maendeleo ya kiuchumi, na kuleta manufaa ya kijamii na kimazingira.
Je, wajua: Uwekezaji katika sekta ya afya na mifumo ya tahadhari za mapema hutoa faida kubwa zaidi kwa kulinda maisha, miundombinu na tija ya kiuchumi.
Sekta ya viwanda inaweza kupunguza asilimia 11 ya uzalishaji wa hewa chafu inayosababishwa na nishati Ulimwenguni Kufikia 2030 kupitia njia za matumizi sahihi ya Nishati
Sekta ya viwanda hutumia kiasi kikubwa cha nishati, hasa kutoka kwenye mafuta. Hivyo, matumizi ya nishati ya viwandani yanachangia takribani robo ya uzalishaji wa hewa chafu duniani.
Ingawa baadhi ya matumizi ya viwandani yanahitaji joto la juu sana (jambo linaloleta changamoto kuondokana na matumizi ya mafuta kwa sasa), kuongeza ufanisi wa nishati kunaweza kupunguza gharama na kupunguza uzalishaji wa hewa chafu duniani kwa asilimia 11 ifikapo 2030.
Je, wajua: Ikiwa matumizi sahihi ya nishati itaongezeka maradufu katika majengo, viwanda na kwenye vyombo vya usafiri ifikapo 2030, hewa chafu itapungua kwa takriban asilimia 30, Hii ni hatua muhimu kuelekea kutokuwa na uzalishaji kabisa wa kaboni ifikapo mwaka 2050.
Kutokana na Athari za mabadiliko ya tabianchi, mamilioni ya wasichana duniani hawawezi kumaliza miaka 12 ya shule.
Athari za mabadiliko ya tabianchi huchochea haki za usawa wa kijinsia katika nyanja nyingi. Wakati jamii zinapokumbwa na majanga au mabadiliko ya hali ya hewa, familia mara nyingi huamua kuwatoa wasichana shule kutokana na ukosefu wa rasilimali au mzigo wa majukumu ya nyumbani.
Kuhakikisha watoto wote, hususan wasichana, wanapata elimu bora ya miaka 12 katika mazingira yanayobadilika ni msingi wa maendeleo endelevu.
Je, wajua: Kufikia mwaka 2050, mabadiliko ya tabianchi yanaweza kuwasukuma wanawake na wasichana milioni 158 zaidi katika umaskini — idadi hii ni milioni 16 zaidi ya wanaume na wavulana watakaokuwa katika hali kama hiyo.
Takribani tani milioni 13 za plastiki kila mwaka hujikusanya ardhini
Plastiki zipo kila mahali. Ziko kwenye maji tunayokunywa, chakula tunachokula, na hata hewa tunayovuta. Zinahatarisha afya, kuchafua mazingira, na kuua viumbe hai.
Plastiki zinachangia mabadiliko ya tabianchi kwa kutoa hewa chafu katika kila hatua ya mzunguko wake: kuanzia uchimbaji wa mafuta yanayotumika kutengeneza plastiki hadi uteketezaji wa taka za plastiki.
Dunia huzalisha takribani tani milioni 430 za plastiki kila mwaka, nyingi zikitumika mara moja tu na kutupwa.
Kila mwaka, takribani tani milioni 13 za plastiki hujikusanya ardhini, zikiharibu rutuba ya ardhi na kupunguza ukuaji wa mazao. Hatimaye, plastiki hizi hubadilika kuwa chembechembe vinavyoweza kuingia kwenye maji na chakula tunachotumia.
Je, wajua: chembechembe za plastiki zina madhara makubwa kiafya — zinahusishwa na saratanı, matatizo ya moyo, uzazi, na magonjwa mengine. Wanasayansi wanakadiria kuwa mtu mzima anaweza kula hadi kipande cha plastiki kinacholingana na kadi ya benki kila wiki.
Sekta ya Usafirishaji, inachangia karibu asilimia 14 ya uzalishaji duniani, ni fursa kubwa ya kuchukua hatua
Sekta ya usafirishaji ni miongoni mwa vyanzo vikuu vya hewa chafu duniani. Ili kupunguza athari zake, nchi zinapaswa kuwekeza katika mifumo ya usafiri endelevu kama vile vibaraza vya kutembea na kuendesha baiskeli, usafiri wa umma wenye utoaji mdogo wa hewa chafu, magari ya umeme yanayotumia nishati safi, na meli na ndege zenye ufanisi zaidi wa nishati.
Zaidi ya kupunguza uzalishaji, usafiri endelevu pia huchangia afya bora, fursa za kiuchumi na uhifadhi wa mazingira.
Je, wajua: Magari ya umeme yaliwakilisha zaidi ya asilimia 20 ya mauzo yote ya magari mwaka 2024, na kiwango hiki kinatarajiwa kufikia asilimia 25 mwaka 2025.
Nishati ya jua na upepo Inachangia asilimia 15 ya nishati ya Umeme Duniani. Kiwango Hiki Kitazidi Maradufu Kufikia 2030.
Mabadiliko kutoka mfumo wa nishati unaotegemea mafuta kwenda kwenye nishati mbadala ni hatua muhimu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Mwaka 2024, nishati mbadala ilichangia karibu asilimia 33 ya nishati ya umeme duniani. Kati ya hizo, upepo na jua zilichangia asilimia 15, huku umeme wa maji na vyanzo vingine vikichangia asilimia 17.
Nishati ya umeme wa jua na upepo ni nafuu zaidi kwa asilimia 41 na 53 mtawalia kuliko nishati ya mafuta, na hivyo kuwa vyanzo vinavyokua kwa kasi zaidi katika historia. Inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2030, mchango wake utaongezeka zaidi ya mara mbili, na kusaidia jamii kuwa endelevu na zenye ustahimilivu zaidi.
Je, wajua: Mwaka 2024, zaidi ya asilimia 92 ya uwezo mpya wa uzalishaji umeme duniani ulitokana na nishati mbadala. Hata hivyo, dunia inapaswa kuharakisha zaidi ili kufikia lengo la kuongeza mara tatu uwezo wa nishati mbadala kufikia mwaka 2030.
Kati ya mwaka 2000 na 2019, hasara zilizotokana na mabadiliko ya tabianchi Zilikadiriwa kufikia dola za marekani nilioni 16 kila saa.
Kadri athari za mabadiliko ya tabianchi zinavyozidi kuongezeka, wanasayansi wamekuwa wakitathmini ni kiasi gani cha uharibifu wa hali mbaya ya hewa kinachosababishwa moja kwa moja na mabadiliko haya.
Utafiti mmoja uliochambua matukio 185 ya hali mbaya ya hewa kati ya mwaka 2000 na 2019, uligundua kuwa hasara za kila mwaka zilifikia wastani wa dola bilioni 143, sawa na dola milioni 16 kwa saa moja. Kwa kuwa takwimu kutoka nchi maskini zilikuwa pungufu, inaaminika kuwa takwimu hizi ni chini ya makadirio halisi..
Je, wajua: Baadhi ya hasara za mabadiliko ya tabianchi haziwezi kupimwa kwa fedha. Hii inahusisha upotevu usio wa kiuchumi kama vile urithi wa kitamaduni, kuhamisha watu kutokana na maafa, au athari za kisaikolojia.
Zaidi ya asilimia 17 ya ardhi na vyanzo vidogo vya Maji zinalindwa
Shughuli za binadamu katika karne iliyopita zimeleta sio tu mabadiliko ya tabianchi bali pia kuporomoka kwa kasi kwa bioanuwai. Changamoto hizi mbili — mabadiliko ya tabianchi na ya asili — zinashabihiana kwa karibu.
Maeneo yaliyohifadhiwa ni muhimu kwa kulinda mazingira na bioanuwai, na yanachangia kupunguza kasi ya mabadiliko ya tabianchi. Mwaka 2022, nchi zilikubaliana juu ya Mfumo wa Kimataifa wa Kunming–Montreal wa Bioanuwai, unaolenga kulinda asilimia 30 ya ardhi na bahari kufikia 2030. Hadi sasa, zaidi ya asilimia 17 ya ardhi na vyanzo vidogo vya maji vimehifadhiwa.
Je, wajua? Pamoja na kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya tabianchi kwa jamii, suluhisho zinazozingatia mazingira (nature-based solutions) zinaweza kuchangia hadi asilimia 37 ya upunguzaji wa hewa chafu kufikia malengo ya Mkataba wa Paris kufikia mwaka 2030.
Mwaka 2024, misitu ya kitropiki sawa na Viwanja 18 vya mpira wa miguu ilipotea kila dakika.
Misitu inafunika takribani asilimia 30 ya uso wa Dunia, sawa na hekta bilioni 4. Ni muhimu kwa uhai wa binadamu kwani hutoa oksijeni, chakula, dawa, na husaidia kufyonza hewa ya ukaa.
Hata hivyo, misitu inakabiliwa na hatari kubwa inayosababishwa na ukataji miti ovyo, upa
nuzi wa kilimo, miji, na moto wa misitu unaoongezeka kutokana na mabadiliko ya tabianchi.
Mwaka 2024, Dunia ilipoteza hekta milioni 6.7 za misitu ya asili ya kitropiki — sawa na viwanja 18 vya mpira wa miguu kwa kila dakika — jambo lililoathiri bioanuwai, uhifadhi wa kaboni, na maisha ya mamilioni ya jamii nyingi zinazotegemea misitu.
Je, wajua: Takribani watu bilioni 1, wakiwemo watu wa jamii asili milioni 70, wanategemea misitu kwa riziki zao. Misitu yenye afya inadhibiti mvua, huzuia mafuriko na mmomonyoko wa udongo, na hutoa maji safi.
Hapa duniani zaidi ya asilimia 19 ya chakula kwenye maduka, migahawa na majumbani kinatumika vibaya
Sekta ya kilimo ni miongoni mwa vyanzo vikubwa vinavyochochea mabadiliko ya tabianchi ikichangia asilimia 33 ya hewa hizo. Pia inatumia asilimia 70 ya maji safi, inachangia mmomonyoko wa udongo, na ni chanzo kikuu cha kupotea kwa bioanuwai.
Pamoja na yote, asilimia 33 ya chakula kinachozalishwa duniani hutumiwa vibaya, ambapo asilimia 13 hupotea kwenye mnyororo wa usambazaji (kutoka shambani hadi sokoni), na asilimia 19 hupotezwa majumbani, madukani na migahawani.
Je, wajua: Upotevu wa chakula ni mzigo mkubwa wa kimazingira lakini pia ni fursa iliyopotezwa ya kulisha watu milioni 783 wanaokabiliwa na njaa duniani kote.
Maji safi yanayopatikana kwa kila mtu yamepungua kwa asilimia 20 ndani ya miongo iliyopita
Maji yako katikati ya changamoto ya mabadiliko ya tabianchi. Kadri hali ya hewa inavyobadilika, mvua haitabiriki, barafu za milimani huyeyuka haraka, na matukio hatari kama mafuriko, dhoruba na ukame huongezeka.
Haya yote yanaathiri kiasi cha maji safi yanayopatikana kwa binadamu ambayo ni asilimia 0.5 pekee ya maji yote duniani. Katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, upatikanaji wa maji safi kwa kila mtu umepungua kwa asilimia 20.
Baadhi ya maeneo duniani yanakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji, jambo linaloweza kuchochea migogoro na ushindani wa rasilimali.
Je, wajua: Zaidi ya watu bilioni 2 wanaishi katika nchi zenye uhaba wa maji, na karibu nusu ya watu wote duniani wanapata uhaba mkubwa wa maji kwa angalau mwezi mmoja kila mwaka.
Gharama za athari ya mabadiliko ya tabianchi kwa afya inaweza Kufikia dola trilioni 21 katika nchi za kipato cha chini na kati kufikia 2050.
Changamoto za mabadiliko ya tabianchi huleta changamoto katika sekta ya afya. Kuanzia joto kali, uchafuzi wa hewa, kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza, hadi uhaba wa chakula na maji, mabadiliko ya tabianchi yanaathiri moja kwa moja afya ya binadamu.
Athari hizi zinachochea ukosefu wa usawa wa kijamii na kiafya kati ya nchi tajiri na maskini. Nchi za kipato cha chini na cha kati ndizo zinazoathirika zaidi, na ifikapo mwaka 2050, gharama za kiafya zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi katika nchi hizi zinakadiriwa kufikia dola za Marekani trilioni 21.
Je, wajua: Mabadiliko ya tabianchi yanaongeza hatari ya kuzuka kwa magonjwa mapya na ya milipuko. Kadri joto linavyoongezeka, mbu wanaobeba malaria na dengu wanaweza kuenea hadi maeneo ambayo awali hayakuwa na magonjwa hayo — na ifikapo mwaka 2070, watu bilioni 4.7 zaidi wanaweza kuwa hatarini.
Uchumi rejeshi unaweza kutengeneza zaidi ya ajira milioni 22 barani afrika, Amerika ya kusini na umoja wa ulaya kufikia mwaka 2030
Uchumi rejeshi unalenga kubadili mifumo isiyo endelevu ya uzalishaji na matumizi kwa kupunguza taka, kutumia upya bidhaa, na kuhifadhi rasilimali asilia.
Njia hii inaweza kutumika katika sekta zote — kutoka kilimo, viwanda, ujenzi hadi mavazi — na kutengeneza mamilioni ya nafasi mpya za ajira. Ifikapo mwaka 2030, uchumi rejeshi unaweza kutengeneza ajira milioni 11 barani Afrika, milioni 8.8 Amerika ya Kusini na Karibiani, na milioni 2.5 katika Umoja wa Ulaya.
Je, wajua: Ni chini ya asilimia 7 pekee ya malighafi duniani inayorejeshwa kutumika tena baada ya matumizi. Kupitisha mbinu za uchumi rejeshi kunaweza kupunguza uzalishaji wa hewa chafu, kulinda asili, na kufungua fursa mpya za kiuchumi.
Viwango vya bahari duniani vimepanda kwa sentimita 23 tangu mwaka 1880
Kuongezeka kwa joto duniani kunasababisha kuyeyuka kwa barafu za milimani, na kuongezeka kwa ujazo wa maji baharini. Tangu mwaka 1880, viwango vya bahari duniani vimepanda kwa sentimita 23, hali inayotishia miji na jamii za pwani duniani kote.
Kupanda kwa kiwango cha maji baharini kunasababisha mafuriko, mmomonyoko wa ardhi, na kuingia kwa chumvi kwenye maji safi, jambo linaloharibu miundombinu, kilimo, na utalii, na kusababisha watu kuhama makazi yao.
Visiwa vidogo viko hatarini zaidi. Hata katika hali ya sasa, mataifa ya Pasifiki yanatarajiwa kushuhudia ongezeko la angalau sentimita 15 zaidi katika miaka 30 ijayo. Baadhi ya ardhi katika visiwa vinaweza kuzama chini ya maji.
Je, wajua: Karibu watu milioni 22 wanaishi chini ya mita 6 kutoka usawa wa bahari, na zaidi ya nusu ya miundombinu katika mataifa mengi ya visiwa iko ndani ya mita 500 kutoka pwani — jambo linaloongeza hatari maradufu.
Tahadhari ya awali ndani ya masaa 24 kabla ya tukio la hali mbaya ya hewa inaweza kuokoa maisha na kupunguza hasara kwa asilimia 30.
Tahadhari za mapema hutoa taarifa muhimu na za wakati kuhusu majanga yanayokaribia kutokea kama vimbunga, mafuriko, ukame, mawimbi ya joto au moto wa misitu.
Taarifa hizi huwezesha jamii kuchukua hatua mapema, kuokoa maisha na kupunguza hasara za kiuchumi. Tahadhari inalotolewa angalau saa 24 kabla ya tukio inaweza kupunguza uharibifu kwa hadi asilimia 30.
Je, wajua: Uwekezaji wa dola milioni 800 pekee katika mifumo ya tahadhari za mapema katika nchi za kipato cha chini na cha kati unaweza kuzuia hasara ya kati ya dola bilioni 3 hadi 16 kila mwaka.
Asilimia 25 ya ardhi duniani inasimamiwa na jamii asili
Jamii za asili zinasimamia takribani asilimia 25 ya ardhi yote duniani, zikiwa walinzi wa asilimia 36 ya misitu hai zaidi duniani. Misitu hii ina kiwango cha chini zaidi cha ukataji miti na uharibifu, na inaendelea kuwa vyanzo muhimu vya kufyonza kaboni — hivyo kuchangia katika kupunguza mabadiliko ya tabianchi.
Kwa kulinda mifumo hii ya ikolojia, jamii hizi zinatoa huduma muhimu kwa mazingira ya dunia nzima, ingawa mchango huu mara nyingi hautambuliwi vya kutosha. Zinastahili ulinzi wa kisiasa na msaada wa kifedha zaidi.
Je, wajua: Suluhisho asilia na uchumi rejeshi ni sehemu ya maisha ya jamii asili na taarifa hii ni muhimu kwa maamuzi juu ya mabadiliko ya tabia nchi.
Asilimia 26 ya watu duniani hawana la kupata nishati safi za Kupikia
Upatikanaji wa njia salama za kupikia si suala la nishati pekee — ni suala la afya, jinsia, na haki za binadamu.
Wakati upatikanaji wa umeme umeongezeka duniani, bado karibu watu bilioni 2.3 ama asilimia 26 ya idadi ya watu duniani wanatumia nishati duni kama kuni na mkaa kwa ajili ya kupikia. Mbali na kusababisha ukataji miti na uharibifu wa misitu, moshi unaotokana na nishati hizi unasababisha vifo vya mapema vya zaidi ya watu milioni 3.7 kila mwaka — wengi wao wakiwa wanawake na watoto.
Zaidi ya hayo, muda mwingi unaotumika na wanawake kukusanya kuni kila siku unapunguza fursa zao za elimu, ajira, na uhuru wa kiuchumi.
Je, wajua: Kuondokana na matumizi ya majiko ya kuni na mkaa na kutumia majiko safi kunaweza kuzuia vifo 463,000 na kuokoa dola bilioni 66 za gharama za afya kila mwaka barani Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.
Kesi ya kihistoria iliyowasilishwa na wanafunzi 27 kutoka visiwa vya pasifiki ilithibitisha wajibu wa kisheria wa nchi kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi
Katika maamuzi ya kihistoria yaliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Haki iliamuru kuwa nchi zina wajibu wa kulinda mazingira kukabiliana na hewa chafu ambayo husababisha mabadiliko ya tabia nchi.
Kesi hii inasemwa kuwa ni ya kihistoria iliyowasilishwa na wanafunzi 27 kutoka visiwa vya Pasifiki chini ya uongozi wa taifa la Vanuatu. Ilisifiwa kama ni ushindi kwa mazingira na nguvu ya vijana katika kuleta mabadiliko.
Je, wajua: Hadi kufikia Disemba 2022, kulikuwa na kesi 2,180 zinazohusiana na mabadiliko ya tabianchi katika sehemu 65 duniani kote, zikiashiria kuongezeka kwa matumizi ya mahakama kama njia ya kutafuta haki za
kimazingira.
Bei ya kaboni inafidiatakribani ya uzalishaji wa hewa chafu duniani.
Upangaji wa Bei ya kaboni ni chombo muhimu cha kiuchumi kinachoweka thamani halisi ya uharibifu unaosababishwa na uzalishaji wa hewa chafu.
Kwa kufanya hivyo, kinahamisha mzigo wa gharama kutoka kwa jamii kwenda kwa wale wanaochafua mazingira.
Mfumo huu ndio msingi wa masoko ya kaboni, ambapo kupunguzwa kwa uzalishaji kunaweza kuuzwa kama hisa za kaboni (carbon credits).
Kwa sasa, takribani asilimia 28 ya uzalishaji wa hewa chafu duniani inafunikwa na bei ya moja kwa moja ya kaboni, jambo linalosaidia nchi kuhamasisha fedha kwa maendeleo endelevu.
Je, wajua: Mapato kutoka bei ya kaboni yalizidi dola bilioni 100 katika mwaka wa 2024. Zaidi ya nusu ya fedha hizi zilitumika kufadhili miradi ya mazingira, miundombinu, na maendeleo.
Asilimia 29 ya aina zote za viumbe duniani ziko hatarini kutoweka kufikia 2100 ikiwa uchafuzi wa mazingira utabaki kuwa juu.
Mabadiliko ya tabianchi yanasababisha mabadiliko yasiyoweza kurekebishwa katika bioanuwai. Kuongezeka kwa joto, mabadiliko ya mvua, na misimu mirefu ya moto wa misitu kunabadilisha makazi ya viumbe na kuathiri usawa wa mifumo ya ikolojia.
Matokeo yake viumbe kadhaa viko katika hatari ya kutoweka, na idadi hii inakisikiwa kuongezeka kama hali ya joto itakuwa zaidi ya nyuzijoto 5. Katika hali ya nyuzijoto 5 zaidi ya asilimia 29 ya viumbe wote duniani wako katika hatari kubwa ya kutoweka.
Je, wajua: Mabadiliko ya tabianchi na uharibifu wa makazi — yote yakisababishwa na shughuli za binadamu — yanaendesha kile kinachoitwa kutoweka kwa wingi kwa sita duniani. Tukio la mwisho kama hili lilitokea takribani miaka milioni 65.5 iliyopita, wakati tendaguru walipotoweka.
Takribani nusu ya watu duniani wako chini ya miaka 30 – mustakabali wao lazima uwe salama, haki na bila uchafuzi wa hali ya hewa.
Watoto na vijana walio chini ya miaka 30 ni karibu nusu ya idadi ya watu duniani. Mabadiliko ya tabianchi yataathiri maisha yao kwa kila njia — mahali watakapokaa, elimu watakayopata, ajira watakazofanya, na hata kama wataweza kuwa familia zao.
Vijana wengi wanafahamu kwamba hatua lazima zichukuliwe kwa haraka na kwa kiwango cha dunia nzima. Wanaongoza harakati za kijamii, kushiriki katika mazungumzo ya kimataifa ya tabianchi, na kubuni suluhisho za ubunifu zinazobadili jamii.
Viongozi na watunga sera duniani wana jukumu la kusikiliza sauti za vijana na kuchukua hatua madhubuti kulinda mustakabali wao. Binadamu hawawezi kustawi kwenye sayari inayoharibiwa na mabadiliko ya tabianchi. Uchumi wa mafanikio ya kesho ni ule unaochukua hatua bunifu za kukabiliana na mabadiliko tabianchi leo.
Baada ya zaidi ya miaka 30 ya mazungumzo ya tabianchi, sasa ni wakati wa kujitolea kikamilifu kwa mustakabali salama, wa haki, na usio na kaboni. Kwa sababu katika kila kipengele cha maisha yetu na cha watoto wetu — #TabianchiNiJamboMuhimu (#ClimateCounts).