Mdahalo wa Kitaifa Kuhamasisha Malipo ya Kidijitali kwa Biashara za Mipakani

March 31, 2026
Group photo of people posing on a stage in front of a blue backdrop.

Washiriki katika Mdahalo wa Kitaifa kuhusu Malipo ya Kidijitali kwa Biashara za Kuvuka Mipaka, ulioandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), UNDP Tanzania na Better Than Cash Alliance, jijini Dar es Salaam.

UNDP Tanzania

Dar es Salaam, 31 Machi 2026

Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwa kushirikiana na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Tanzania na Jumuiya ya Kimataifa ya Matumizi ya Malipo ya Kidijitali (BTCA), imeandaa mdahalo wa kitaifa wenye lengo la kuimarisha matumizi ya malipo ya kidijitali kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati (MSMEs) wanaofanya biashara za kuvuka mipaka ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Lengo la mdahalo huu ni kuwaleta pamoja wadau wakuu ili kupitia matokeo ya tafiti zilizofanywa mipakani maeneo ya Namanga, Mutukula, Rusumo na maeneo makuu ya biashara ikiwemo Arusha, Bukoba na Mwanza; kutambua changamoto zao, kukubaliana hatua za kipaumbele, na kuweka mkakati wa utekelezaji wa suluhisho za malipo ya kidijitali zilizo salama, nafuu na jumuishi.

Mdahalo huu unawakutanisha wadau mbalimbali kutoka sekta ya umma na binafsi, wakiwemo,Wizara ya Viwanda na Biashara, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Idara ya Uhamiaji, Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), taasisi za fedha, watoa huduma za fedha kwa njia ya simu,Umoja wa chama cha mabenki Tanzania, Umoja wa wanachama wa huduma za fedha kwa njia ya simu (TAMNOA),  Umoja wa Taasisi za Teknolojia ya Fedha (TAFINA)), vyama vya wafanyabiashara wa mipakani, pamoja na makundi ya wanawake na vijana.

Licha ya kuongezeka kwa matumizi ya huduma za kifedha, biashara nyingi za mipakani bado zinafanyika kwa fedha taslimu kutokana na changamoto kama ada kubwa na zisizo wazi za miamala, ukosefu wa muingiliano wa mifumo ya malipo, changamoto za ubadilishaji fedha za kigeni, kushindwa kukamilika kwa miamala, pamoja na masharti magumu ya utambuzi wa wateja (KYC). 

Mdahalo huu unatarajiwa kuleta uelewa wa pamoja wa changamoto hizo, kubainisha vipaumbele vya kitaifa, na kuandaa mpango kazi wenye mkakati mahsusi  wa utekelezaji. Aidha, utachangia maandalizi ya mchango wa Tanzania katika Mpango wa Kikanda wa Malipo ya Kuvuka Mipaka wa EAC.

Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwa kushirikiana na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) na Jumuiya ya Kimataifa ya Matumizi ya Malipo ya Kidijitali (BTCA), wanaendeleza ushirikiano wa kimkakati unaolenga kuharakisha ujumuishaji wa kifedha na kukuza uchumi wa kidijitali nchini. Kupitia jukwaa la BTCA, UNDP inawezesha ubia kati ya sekta ya umma na binafsi ili kuhamasisha matumizi ya teknolojia, ubunifu na uwekezaji katika suluhisho za malipo ya kidijitali zilizo salama, nafuu na jumuishi, huku BoT ikiendelea kuweka na kusimamia sera na mifumo inayohakikisha usalama, uthabiti na ufanisi wa sekta ya fedha. Ushirikiano huu unalenga kurahisisha miamala ya ndani na ya kuvuka mipaka, kupunguza utegemezi wa fedha taslimu, na kuwezesha wafanyabiashara pamoja na makundi yaliyo pembezoni kunufaika kikamilifu na fursa za uchumi wa kidijitali, hivyo kuchochea ukuaji wa uchumi endelevu nchini na katika ukanda wa Afrika Mashariki.